Luke Shaw amekemea kiwango cha Manchester United kwa kupokea kichapo cha 3-1 dhidi ya West Ham kwa kukielezea kwamba ni kibovu ' cha kutisha ' lakini amegoma kumlaumu kocha Jose Mourinho.
United wapo nyuma dhidi ya vinara Manchester City ambao wapo sawa na Liverpool kwa tofauti ya Pointi tisa wakiwa wamepoteza mechi tatu za kwanza kati ya saba za Ligi.
" Kama unataka ukweli nafikiri kilikuwa kiwango kibovu cha kutisha. Hatukuonekana timu ambayo ilikuwa inaweza kumfunga West Ham . Nafikiri mchezaji mmoja mmoja na timu kwa ujumla tulikuwa ovyo."
"Kiwango kile hakitoshi ni ngumu kukubali na tunaomba msamaha kwa mashabiki kwa kile walichokiona. Kiwango cha chini sana kulinganisha na wachezaji wenye vipaji ndani ya Manchester United."
Shaw amesema kwamba Mourinho alitoa maneno ambayo yalikuwa yanahitaji wakati wa mapumziko , na kusisitiza kwamba wachezaji ndio wanastahili kulaumiwa na sio kocha wao.
"Ni wazi wakati wa mapumziko kulikuwa na maneno kadhaa makali na naamini yalihitajika kusemwa. Ilikuwa kutuamsha kwamba tunahitajika kucheza zaidi mpira na hiyo haikutokea, inasikitisha."
"Inabidi tujiangalie wenyewe kama wachezaji . Sisi ndio tunaokwenda uwanjani . Kocha hayupo uwanjani au sio ? Yeye yupo pale kupanga timu , timu ambayo anaamini italeta ushindi . Ukiangalia timu yetu leo ilikuwa imara sana, hakuna visingizio . Kama wachezaji tulivurunda."
0 comments:
Post a Comment