Beki wa Yanga Andrew Vincent Chikupe ‘Dante’ amesema taarifa za nahodha wa Simba, John Bocco kuukosa mchezo wa Septemba 30 ni habari njema kwao, lakini akafichua anamjua vyema Emmanuel Okwi na anataka kumsoma zaidi Meddie Kagere akitenga muda maalumu wa kufanya hivyo.
Dante ambaye yuko kambini mkoani Morogoro na kikosi cha Yanga amesema Bocco ni mshambuliaji aliyekamilika na kukosekana kwake katika mechi ya Jumapili wiki hii kutaipunguzia kazi safu yao ya ulinzi.
Dante amesema katika mastraika wa Simba waliosalia wote anawajua vyema na jinsi ya kuwazuia, lakini ni Kagere pekee anataka kumsoma zaidi akimtengea siku tatu sawa na masaa 72 za kumfuatilia.
Beki huyo alisema mbinu za kumzuia Okwi zipo ndani ya uwezo wao, ila atatumia muda wa siku tatu kujiongeza ili kujua mbinu za Kagere katika kufunga.
“Tumesikia kwamba Bocco amepata kadi nyekundu ni pigo kwao kutokana na Bocco sio mshambuliaji rahisi anajua kupambana na kufunga.
"Kagere analijua goli pia ana uzoefu aliposajiliwa Simba nilianza kumsoma taratibu, ila kwa siku hizi tatu hizi nataka kazi hiyo.”
0 comments:
Post a Comment