Friday, October 12, 2018

Na Masau Bwire

Baada ya kufungwa na Cape Verde, tusilaumu, tushauri.
Ni kweli, siku zote katika maisha, hakuna asiyetaka mafanikio, wote mafanikio tunayataka, tutayapataje, ndio mtihani.

Wapo ambao mafanikio yao ni kama bahati tu, ahangaiki kuyapata, yanakuja tu, hata kushangaa, amepataje kufanikiwa hivyo, lakini, wapo wanaotaabika, kuhangaika, kupata taabu sana kuyafikia mafanikio, hawa ndio wengi.

Kutafuta mafanikio, ukafanikiwa, njiani lazima ukutane na vikwazo vingi, vingi mno, kijikaza kwako, uvumilivu na kutokukata tamaa ni kufanikiwa kwako.

Ukijikwaa, ukaanguka, nyanyuka, anza safari, ukitafakari, ulijikwaaje mpaka kuanguka ili, usijikwae na kuanguka tena.

Lakini utakapojikwaa na kuanguka, ukafa moyo, ukadhani ni ngumu kusafiri na kufika mwisho wa safari, kweli hutofika kwasababu tayari umejiweka katika hali ya kutokufika.

Kumbukeni pia, mafanikio ya wengine huja kwa wengine kuwatia moyo, akiona mwenzie kateleza, kaanguka, anamtia moyo, kumsihi asikate tamaa, akaze mwendo, avumilie, atafika tu, mwisho wa safari.

Katika maisha, ni vigumu na ni mara chache sana, kufanikiwa bila kukutana na chochote cha kukwaza na kuchelewesha kufanikiwa kwako, ukikutana na hii hali, usikate tamaa, songa mbele, utafanikiwa.

Taifa Stars, imefungwa na mwenyeji Cape Verde goli 3-0, matokeo ambayo yamezua gumzo kila pahali.

Katika mjadala huo, wengine wanasukuma lawama kwa kocha, hawa ndio wengi, wengine lawama wanazipeleka kwa wachezaji, TFF na Serikali, kwamba, kwa namna fulani, ni wasababishi wa matokeo hayo.

Kumbukeni, kocha ni huyo, huyo tulimpongeza tulipokutana na Uganda, tena baada ya kuwaacha wachezaji wengi wenye majina katika soka la Tanzania, lakini leo tunamponda.

Timu yoyote kufungwa ni jambo la kawaida, si kweli kwamba, timu zote zinazokuwa bingwa, huwa hazifungwi mchezo hata mmoja.

Badala ya mjadala uliojiegemeza zaidi kwenye lawama, mimi nashauri, tujielekeze kujadili nini kifanyike ili mchezo unaokuja tufanye vizuri, nafasi bado tunayo, kubwa tu ya kusonga mbele.

Matokeo hayo, tuyachukulie kama changamoto, vikwazo na adha ya kawaida katika safari yetu, ni utelezi umetuteleza na kuanguka, tushikane, tunyanyuane, tusonge mbele, tutafika salama mwisho wa safari yetu tena, kwa mafanikio makubwa.

Tusikatishane tamaa, hatutafika kule tunakostahili kufika kwa kujiwekea ugumu kwenye urahisi sisi wenyewe.

Kufikiri ni kazi....Tufikiri kabla ya kufikiri.....Tufikiri sana baada ya kufikiri.... Na Masau Kuliga Bwire - Mzalendo.

0 comments:

Post a Comment