Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Oktoba 5, 2018 ilipitia taarifa na matukio katika mechi za Ligi Kuu ya Tanzania (TPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zinazoendelea hivi sasa.
Mchezaji Erasto Nyoni wa Simba SC amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumpiga kiwiko Hassan Nassoro Maulid wa Ndanda SC, tukio hilo halikuonwa na Mwamuzi wa mechi hiyo iliyofanyika Septemba 15, 2018 katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Mechi namba 52 (Mwadui FC 1 vs Simba 3). Nahodha John Bocco wa Simba amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga mchezaji wa timu pinzani.
Mechi namba 48 (Mbao FC 1 vs Simba 0). Klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuwarushia chupa za maji na soda viongozi, wachezaji na Kocha Mkuu wa timu yao baada ya mechi hiyo iliyochezwa Septemba 20, 2018 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kumalizika.
Mechi namba 33 (Ndanda SC 0 vs Simba 0). Timu ya Simba imepewa Onyo Kali kwa kutowasilisha orodha ya wachezaji wake (team match list) katika kikao cha maandalizi ya mechi. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 72 (Simba SC 0 vs Yanga SC 0). Mchezaji James Kotei wa Simba anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumpiga ngumi Gadiel Gabriel wa Yanga katika dakika ya 33, tukio ambalo Mwamuzi hakuliona katika mechi hiyo iliyofanyika Septemba 30, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Naye Andrew Vincent wa Yanga anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumpiga kichwa Mohamed Hussein wa Simba katika dakika ya 61, tukio ambalo halikuonwa na Mwamuzi.
0 comments:
Post a Comment