Mshambuliaji wa timu ya Lipuli FC yenye maskani yake Mjini Iringa Malimi Busungu ameibukia mkoani Dodoma na kukanusha madai ya kuondoka kambini bila taarifa.
Azam TV imemsaka mchezaji huyo baada ya uongozi wa Lipuli kudai kuwa haijui mahali aliko baada ya kutojumuika na wachezaji wenzake katika safari ya kuelekea Jijini Mwanza ambako Lipuli ilikwenda kucheza na Mbao FC.
Katika maelezo yake, Busungu ameeleza kuwa awali aliomba ruhusa kuwa alikuwa anaumwa wakati kikosi kilipokwenda kambini mkoani Mbeya, kikosi kiliporejea Iringa, aliungana nacho lakini akapata taarifa kuwa mke wake ambaye yuko Dodoma, ni mgonjwa.
Busungu anasema aliomba ruhusa kwa meneja wa timu hiyo, lakini meneja hakutaka kumsikiliza na ndipo yeye alipoamua kuondoka Iringa na kuelekea Dodoma kwaajili ya kumuuguza mke wake.
Amesema aliporejea Iringa uongozi ulimtaka kwenda kujieleza kwenye Kamati ya Nidhamu lakini yeye aliupa uongozi huo sharti kuwa ili akahojiwe, ni lazima aende na mchezaji mwingine ambaye pia aliondoka kambini bila ruhusa.
Baada ya sharti hilo la Malimi kutotekelezwa, aliamua kurejea Dodoma ambako ndiko aliko hadi sasa.
Kuhusu madai ya kushinda bar akilewa, Malimi amekanusha madai hayo akidai kuwa anafanyiwa fitna.
Katika hatua nyingine Malimi pia amesisitiza kuwa anaidai timu yake fedha za usajili kiasi cha shilingi milioni 1.5 na mishahara ya miezi miwili mfululizo
0 comments:
Post a Comment