Wachezaji wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam wamegoma kufanya mazoezi leo asubuhi wakishinikiza walipwe malimbikizo ya mishahara yao pamoja na fedha za usajili.
Tukio hilo limetokea asubuhi ya leo Uwanja wa Chuo cha Maafisa wa Jeshi la Polisi, Kurasini, Dar wakati wachezaji walipokutana kwa ajili ya mazoezi ya asubuhi.
Wachezaji wote walifika mazoezini mapema Saa 2:00 asubuhi ya leo, lakini wakawaagiza Manahodha wao, Ibrahim Ajibu na Juma Abdul waende kumuambia kocha Mwinyi Zahera, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwamba hawatafanya.
Na hiyo ni baada ya jana wachezaji hao kumuomba Zahera ambaye pia ni kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya DRC awaite viongozi kwenye mazoezi ya leo asubuhi ili wajadiliane juu ya stahiki zao.
Lakini kitendo cha kutotokea kwa kiongozi hata mmoja mazoezini leo kiliwaudhi wachezaji na kukubaliana kuondoka bila kufanya mazoezi.
Na Kocha Zahera alionyesha msimamo wa kutotaka kujadiliana chochote na wachezaji zaidi ya kuwaamrisha waingie uwanjani kufanya mazoezi. Mwishowe, wachezaji wakaondoka na kocha naye na Maafisa wake wa benchi la Ufundi wakaondoka kinyonge.
Hayo yanatokea siku nne kabla ya mchezo muhimu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Azam FC Jumatatu Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment