Thursday, September 27, 2018

Kamati ya maadili ya chama cha soka mkoa wa Iringa (IRFA) imewafungia baadhi ya wanamichezo mkoani humo kutokana na makosa mbalimbali, mwenyekiti wa kamati ya maadili Musa Mhagama amethibitisha.

Eliud Mvela amefungiwa miaka 5 kujihusisha na masuala ya soka baada ya kukukutwa na hatia kwa makosa mawili, kosa la kwanza ni kushindwa kuheshimu maamuzi ya chama cha soka mkoa wa Iringa (IRFA) kosa la pili ikiwa ni kujipatia faida katika mchakato wa uuzwaji wa iliyokuwa klabu ya Polisi Iringa kinyume na kanuni za shirikisho la soka nchini (TFF).

"Akiwa Katibu wa IRFA alisimamia mchakato wa uuzwaji wa timu ya Polisi Iringa, katika mchakato huo alipata malipo ya ununuzo wa timu hiyo ambayo malengo ilikuwa ni kulipa madeni ambayo klabu hiyo ilikuwa ikidaiwa lakini mlalamikiwa alishindwa kulipa deni wakati tayari malipo ya uuzwaji wa klabu hiyo alikuwa ameshayapata."

Ramadhani Mahano ambaye ni mwenyekiti wa klabu ya Lipuli FC, amefungiwa miaka 8 kujihusisha na soka baada ya kutiwa hatiani kwa makosa matatu (kushindwa kuheshimu maamuzi ya chama cha soka mkoa wa Iringa, kushawishi vilabu kuvunja sheria pamoja na kujivisha cheo ambacho sio chake na kufanya maamuzi kwa udanganyifu).

"Mlalamikiwa alishtakiwa kwa makosa aliyoyafanya akiwa kamishna wa mchezo October 31, 2017 akiwa kamishna wa mchezo katika ligi ya mkoa wa Iringa mechi kati ya Udzungwa Heroes dhidi ya Akosato FC mechi ambayo ilichezwa uwanja wa Ilula Sokoni, alivishawishi vilabu hivyo kucheza mechi bila kuwepo waamuzi wawili wa pembeni."

0 comments:

Post a Comment