Mshambuliaji hatari wa Yanga Heritier Makambo amemtia kiwewe kocha wa Stand United Athumani Bilali 'Bilo' kuelekea mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara baina ya timu hizo utakaopigwa kesho Jumapili kwenye uwanja wa Taifa.
Makambo tayari amepachika bao moja kwenye ligi msimu huu katika mchezo wa kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar huku bao lake jingine likikataliwa na kupelekea mwamuzi wa mchezo huo kufungiwa.
Bilo amesema Makambo ni miongoni mwa washambuliaji bora kwenye ligi na watahitaji kujipanga ili waweze kumdhibiti "Nimewapa kazi maalumu walinzi wangu kuhakikisha wanatembea nae popote aendapo ili asilete madhara," amesema Bilo
Makambo ndio mshambuliaji anayeogopwa zaidi na walinzi wa timu pinzani kwenye ligi ambapo baada ya kuonyesha kiwango cha hali ya juu amekuwa akikamiwa sana.
Kwenye moja ya mahojiano yake Makambo alisema walinzi wa timu pinzani wamekuwa wakimkamia na kumfanyia rafu kwa lengo la kutaka kumuumiza.
Lakini amesema yeye ni mshambuliaji na alitarajia matukio kama hayo kutoka kwa wapinzani wake. "Mimi kazi yangu ni kupachika mabao. Changamoto ya kukamiwa na walinzi wa timu pinzani nimeizoea na nitandelea kufunga kila nitakapopata nafasi," amesema.
Uwezo wake wa kutumia miguu yote, uhodari katika kumiliki mpira na kufunga kwa kichwa umemfanya kuwa mshambuliaji wa kuogofya kwenye ligi msimu huu
0 comments:
Post a Comment