Monday, October 22, 2018

Kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, raia wa DR Congo, ameweka wazi kuwa siyo ndani ya klabu yake pekee bali ni timu zote za Tanzania hakuna mchezaji mwenye uwezo wa kumzidi.

mshambuliaji wake, Ibrahim Ajibu. Mkongo huyo ameyasema hayo ikiwa ni baada ya Ajibu kuwa na mwenendo mzuri kwenye ligi hadi sasa baada ya kutoa pasi nane za mabao ‘asisti’ pamoja na kufunga mabao matatu katika mechi saba alizoichezea Yanga.

Zahera ambaye ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya DR Congo, amesema kwamba Ajibu amekuwa na uwezo wa kipekee kutokana na uwezo mkubwa wa kufikiria ni wapi atatoa pasi kabla ya kupokea mpira, tofauti na wachezaji wengi ambao wanafanya maamuzi yao baada ya kupokea mpira.

“Hakuna mchezaji kama Ajibu, ana akili nyingi sana, ujue yeye
ana tofauti kabisa na wachezaji wengi ndani ya Tanzania kwani anafanya maamuzi yake kabla ya kupata mpira anakuwa kashaamua ni wapi ataupeleka tofauti na wachezaji wengi sana hapa nchini."

“Siyo tu ndani ya Yanga ila nimeangalia timu zote za Tanzania hakuna ambaye anamfikia kwa uwezo lakini shida yake ni moja tu hajitoi kabisa kwa ajili ya timu, yeye anacheza bila ya kutumia nguvu nyingi sana jambo ambalo linamfanya asiwe mzuri wakati timu inapokuwa inashambuliwa,” alisema Zahera.

0 comments:

Post a Comment