Matokeo ya sare dhidi ya Singida United na baadae Mbeya City ndiyo iliyoiondoa rasmi Yanga kwenye mbio za ubingwa msimu huu.
Yanga iliutema rasmi ubingwa wa VPL siku ilipolazimishwa sare ya bao 1-1 na Mbeya City kwenye mchezo ambao ulijaa kila aina ya vituko.
Uwanja wa Sokoine uligeuzwa kuwa uwanja wa vita!
Kwenye mchezo huo tulishuhudia mashabiki wa Mbeya City wakiwapiga mawe wachezaji wa Yanga hasa mlinda lango Youthe Rostand aliyelazimika kulikimbia lango mara kadhaa ili kunusuru maisha yake.
Jeshi la Polisi lilitumia mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki wa Mbeya City waliokuwa wakirusha mawe uwanjani.
Wakati mchezo ukielekea ukingoni ikashuhudiwa tena Mbeya City wakicheza 11 uwanjani licha ya kuwa mchezaji mmoja alikuwa ametolewa nje kwa kadi nyekundu.
Baada ya michezo hiyo Yanga imeshindwa kurudi kwenye kiwango chake na kujikuta ikicheza sasa michezo tisa bila ya kupata ushindi.
Sawa, kuna wakati morali ya wachezaji ilishuka hasa baada ya kupoteza ubingwa ukichanganya na changamoto zinazowakabili klabuni.
Lakini kikosi hiki cha Yanga kinaenda kuandika historia 'mbaya' ya kucheza michezo mingi bila ya kushinda.
Thomas Kipese, mmoja wachezaji waliowahi kuitumikia Yanga, katika mahojiano yake na gazeti moja la kila siku anasema hana kumbukumbu ya kuwahi kuishuhudia Yanga ya aina hii. "Sijawahi kuona hivi. Yanga siyo timu ya kutopata ushindi mechi nyingi mfululizo hivyo. Mimi nazijua Simba na Yanga. Simba imeshawahi kuwatokea mara nyingi, lakini Yanga ni timu ambayo ikifungwa leo, mechi ijayo itashinda, ikitoka sare mechi moja na nyingine ikifungwa inayofuata itashinda." Lakini mwaka huu hali imekuwa tofauti Yanga imefungwa michezo minne mfululizo ya ligi kuu ya Vodacom.
Yaani katika michezo tisa iliyopita, Yanga imefungwa michezo sita na kuambulia sare michezo mitatu pekee.
Yanga inalazimika kushinda michezo yake mitatu ya ligi iliyobaki ili kurejesha imani ya mashabiki wake.
Kuendelea kucheza mda mrefu bila kushinda kutaishusha thamani ya klabu mara dufu na huenda ikawa na wakati mgumu sana kurejesha ule utawala wake.
Moja ya changamoto inayoikumba Yanga sasa ni kutokuogopwa na wapinzani wake.
0 comments:
Post a Comment