Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amepanga kukutana na Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Yanga Hussein Nyika ili kujua maendeleo ya mchakato wa usajili.
Dirisha la usajili linatarajiwa kufungwa wiki ijayo Julai 06, mpaka sasa Yanga ikiwa imesajili wachezaji sita.
Zahera amechukizwa na kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya Gor Mahia juzi ambapo jana baada ya Yanga kurejea aliwaambia waandishi wa habari kuwa timu hiyo inahitaji mabadiliko makubwa ya kikosi chake. “Hapana. Ni lazima tufanye kitu cha maana, ninapaswa kukutana na viongozi wa Kamati ya Usajili, kuna haja ya kukijenga kikosi upya,” Zahera amenukuliwa na gazeti la Mwanaspoti. “Kwanza nataka wafanye haraka usajili wa wachezaji niliowapendekeza kulingana na maeneo husika, hii itasaidia kuirudisha timu katika hali yake. "Pia wachezaji muhimu waliomaliza mikataba nao washughulikiwe, wana msaada mkubwa ndani ya timu, sitapenda kusikia wanaondoka. “Mabadiliko ya timu hasa kwa wachezaji wapya ni muhimu, ni lazima kufanya hivyo haraka, ingawa hawatatumika katika mashindano haya.” Zahera alisema wamepoteza mechi ya Gor Mahia kwa sababu timu haikuwa pamoja kwa muda mrefu. “Nitawaomba viongozi tusivunje kambi ili tukae pamoja kujenga timu na kurekebisha makosa yaliyojitokeza,” aliongeza Zahera.
Katika hatua nyingine Zahera ametaka wachezaji Mrisho Ngassa, Deus Kaseke na straika Heririer Bakambo masuala yao na CAF yakamilishwe haraka iwezekanavyo.
Katika usajili wa dirisha dogo wa CAF ambao Yanga walitakiwa kuongeza majina matatu, walichelewa kutuma majina hayo kwa sababu kuna mambo hawakukamilisha.
“Naomba viongozi wafanyie kazi hilo kwa haraka kwani tukiwatumia wachezaji hawa katika mechi ijayo na Gor Mahia itakuwa vizuri, wanaweza kuongeza kitu katika timu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment