Wednesday, September 26, 2018

Jumapili ijayo, Septemba 30, 2018 watani wa jadi Yanga na Simba wanashuka kwenye uwanja wa Taifa kucheza mchezo wa 98 baina ya timu hizo tangu mwaka 1965 katika ligi.

Simba itakuwa mwenyeji wa mchezo huo ambao ni wa kwanza baina ya timu hizo msimu huu.

Yanga ndio timu yenye mafanikio zaidi katika mchezo wa watani wa jadi ikiwa imejikusanyia jumla ya alama 114, imeshinda michezo 36, sare 34 na kupoteza mara 27.

Simba ina alama 87, imeshinda michezo 27, imetoka sare michezo 34 na kufungwa mara 36.

Hata hivyo misimu ya hivi karibuni Simba imekuwa ikitawala zaidi 'Kariakoo Derby'. Zahera apania kurejesha ubabe wa Yanga

Msimu uliopita haukuwa mzuri kabisa kwa Yanga ambayo ilikumbwa na changamoto ya kiuchumi na kuwapa nafasi wapinzani wao Simba kutawala.

Yanga iliambulia alama moja pekee kwenye mchezo kati yake na Simba ikitoka sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa mzunguuko wa kwanza na kufungwa 1-0 kwenye mchezo wa mzunguuko wa pili.

Kwa ujumla katika misimu miwili iliyopita, Yanga haijafanikiwa kuifunga Simba kwani msimu wa 2016/17 nao mchezo wa mzunguuko wa kwanza ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 huku Simba ikishinda 2-1 kwenye mchezo wa mzunguuko wa pili.

Mara ya mwisho kwa Yanga kuifunga Simba ilikuwa msimu wa 2015/16 ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye michezo yote miwili ya ligi.

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amepania kuandika rekodi mpya kwa kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa Jumapili.

Hans van Pluijm ndiye kocha wa mwisho kuipa ushindi Yanga dhidi ya Simba misimu miwili iliyopita.

George Lwandamina mpaka anaondoka mwishoni mwa msimu uliopita, hakuweza kupata ushindi dhidi ya Simba.

Lakini kikosi cha Yanga sasa chini ya Zahera kimeimarika kikiwa tayari kimeibuka na ushindi kwenye michezo yake yote minne ya ligi.

Zahera amefanikiwa kurejesha ule utamaduni wa soka la Yanga la kushambulia kwa kasi kwa kutumia viungo na washambuliaji wa pembeni.

Utamaduni huo ulipoa wakati wa kocha George Lwandamina ambaye alipendelea zaidi soka la kujihami na kushambulia kwa kushitukiza.

0 comments:

Post a Comment