Tuesday, September 18, 2018

Uongozi wa Yanga umemkingia kifua kipa wake, Mkongomani, Klaus Kindoki kwa kusema kuwa  hana makosa yoyote, Baada ya kuruhusu kambani mabao matatu kutoka kwa straika hatari wa Stand United

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mashindano, Hussein Nyika, amesema kuwa kilichotokea juzi Uwanjani ni matokeo ya mpira hivyo hakuna haja ya kumtupia lawama Kindoki.

Nyika ametolea ufafanuzi suala la mashabiki wengi wa Yanga kuutaka Uongozi umuweke benchi kipa huyo kuwa halina mantiki kwa maana matokeo hayo yametokana na namna timu mbili zilivyocheza.

Kiongozi huyo amefunguka kuwa timu ilikuwa Uwanjani kwa lengo la kusaka pointi tatu ambapo lengo hilo lilifanikiwa, akieleza si vema kuanza kumtupia lawama kipa wao.

Aidha, Nyika amesema kama mchezaji alifanya makosa si sahihi kuwekwa benchi na badala yake Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera kama mkuu wa benchi la ufundi atarekebisha mapungufu ya kikosi.

Kauli hiyo inakuwa inatoa jibu moja kwa moja kwa baadhi ya mashabiki wa Yanga ambao walianza kuutaka uongozi kumpiga benchi kipa huyo wakidai aliruhusu mabao kiulaini.

0 comments:

Post a Comment