Monday, September 24, 2018

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera ametaja sababu za kutowatumia baadhi ya wachezaji kwenye mchezo wa jana dhidi ya Singida United ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Zahera amesema baadhi ya wachezaji hakuwatumia kutokana na sababu mbalimbali.

"Mimi sipumzishi mchezaji bila sababu. Kamusoko aliumia juzi mazoezini wakati akiwa kwenye harakati za kupiga kona. Ngasa nae ni mgonjwa alipatwa na malaria.

Alianza kuumwa baada ya mchezo dhidi ya Coastal Union."

"Makambo aliumia kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union. Alianza mazoezi jana (juzi) lakini Daktari wa timu akatushauri ni vyema tukampumzisha ili aweze kupona kabisa."

Akizungumzia mabadiliko upande wa mlinda lango, Zahera amesema alimpa Kakolanya nafasi jana baada ya kujiridhisha yuko 'fit'

"Kakolanya sikuweza kumtumia kwenye michezo miwili iliyopita kwa kuwa hakuwa na mazoezi ya kutosha," amesema.
"Alipotoka Uganda na timu ya Taifa alichelewa kuanza mazoezi.

"Lakini pia Kindoki alifanya kosa moja kwenye mchezo dhidi ya Stand United. Kumsaidia kumjenga kisaikolojia ilikuwa ni lazima acheze mchezo dhidi ya Coastal Union."

"Huwezi kumuweka mchezaji nje kisa amefanya kosa moja kwenye mchezo uliopita. Tukianza kufanya hivyo kila siku tutakuwa tunabadilisha timu kwani wachezaji wote wanafanya makosa," amesema  Kocha Zahera.

0 comments:

Post a Comment