Wednesday, December 12, 2018

Kiungo mshambuliaji wa Yanga Emmanuel Martin huenda akatimkia Ruvu Shooting baada ya kushindwa kumshawishi kocha Mwinyi Zahera.

Mkataba wa Martin aliyeitumikia Yanga kwa misimu miwili unaelekea ukingoni na timu hiyo haijaonyesha nia ya kumuongezea mkataba mwingine.

Martin pia anawaniwa na Tanzania Prisons inayopambana ijinusuru kutoka nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi.

Yanga bado haijaweka hadharani majina ya wachezaji iliyowasajili na wale walioachwa wakati huu wa dirisha dogo la usajili ambalo litafungwa Jumamosi Disemba 15 2018

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF mapema jana, timu haitaruhusiwa kusajili wachezaji wapya kama tayari kikosi chake kina wachezaji 30.

Idadi hiyo inahusisha wachezaji waliotolewa kwa mkopo pia.

Yanga huenda ikalazimika kuacha baadhi ya wachezaji ili iweze kusajili kwani kikosi chake tayari kina wachezaji 30.

Wachezaji ambao 'wamekalia kuti kavu' ni wale ambao wamekosa kabisa nafasi kwenye kikosi cha Zahera.

Emmanuel Martin, Pato Ngonyani, Yohana Mkomola na Said Mussa hawajacheza mchezo wowote kwenye ligi

Pato anahusishwa kutimkia African Lyon, wakati Mkomola anadaiwa kuweka ngumu kujiunga na Namungo Fc alikopelekwa kwa mkopo.

0 comments:

Post a Comment