Makambo vs Ambokile vita ya mabao Mbeya
Wakati Yanga ikitua jijini Mbeya mapema leo ikiwa na kikosi chake kamili kikiongozwa na kinara wake wa mabao Heritier Makambo tayari kwa mchezo wa keshokutwa dhidi ya Mbeya City, safu ya ulinzi ya vinara hao wa ligi kuu itapaswa kumchunga mshambuliaji Eliud Ambokile.
Ambokile amekuwa na mwendelezo mzuri wa kupachika mabao ambapo juzi aliifungia Mbeya City mabao manne katika mchezo wa kombe la FA (ASFC) dhidi ya Mgambo Fc.
Makambo na Ambokile ndio wanaongoza orodha ya wapachika mabao kwenye ligi mpaka sasa wakiwa wamefunga mabao tisa wakiwa sawa na Said Dilunga wa Ruvu Shooting.
Ukiachana na vita ya mabao ya washambuliaji hao, mchezo wa keshokutwa unatarajiwa kuwa na ushindani mkali jambo hilo likichangiwa kwa kiasi kikubwa na mazingira magumu inayokumbana nayo Yanga kila inapocheza kwenye uwanja wa Sokoine iwe dhidi ya Tanzania Prisons au Mbeya City.
Katika mchezo huo, safu ya ulinzi ya Yanga inatarajiwa kuongozwa na nahodha Kelvin Yondani na Abdallah Shaibu 'Ninja' huku jina la Andrew Vicent Chikupe likiendelea kukosekana akiwa amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kufuatia matukio yaliyotokea kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons.
Chikupe tayari amekosa michezo miwili, dhidi ya African Lyon na mchezo wa kombe la FA dhidi ya Tukuyu Stars.
Winga Mrisho Ngasa ambaye naye alionyeshwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Prisons amemaliza adhabu yake
Wakati Mbeya City wakimtegemea zaidi Ambokile katika upachikaji mabao, kwa upande wa Yanga hali ni tofauti.
Makambo na Tambwe ndio washambuliaji wafungaji lakini wachezaji wote wa Yanga wamejipambanua kuwa na uwezo wa kufunga, na hii ni moja ya sababu inayoibeba Yanga katika mchezo huo.
Lakini pia Yanga itakuwa na Kocha wake Mkuu Mwinyi Zahera aliyerejea leo kutoka nchini Ufaransa .
Zahera amesema wamepania kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi katika duru ya kwanza hivyo wanahitaji kupata matokeo kwenye michezo miwili iliyobaki wa kwanza ukiwa huu wa Mbeya City na mwingine dhidi ya Azam Fc
0 comments:
Post a Comment